Saturday, July 7, 2012

Mzomo


                 MZOMO

Ninao huzuni moyoni, n’simamapo mbele yenu
Vijana mmeasi, tena hamna adabu
Kama mbuzi mmekuwa, popote mwendapo
Wallahi n’kikupata, utajuta kuzawa kwako!

Kazaliwa kijitoto, kizuri chenye afya
Naye Mola kajaliya, kikawa kisichana
Sasa kwisha baleghe, vijana mwamfatafata
N’tavunja mtu mgongo, wengine wapate somo!

Nimtumapo dukani, sokoni na kwingine
N’kitumai njiani kote, wasiwasi hamna
Vijana mwamfatafata, kama nzi kwa kinonda
N’tang’oa mtu meno, kibogoyo liwe jina!

Njiani apitapo, malkia afadhali
Mbija na kumtizama, vyote huwa ni kwake
Hamwachi kumtizama, hata kwa dakika moja
N’tatoboa mtu macho, atembee kwa kuongozwa!

Binadamu wote sawa, wafaa kuheshimiwa
Mheshimu wasichana, nao tawapa heshima
Kikataa nisikiza, utajuta kuzawa kwako
Utajuta ngalijuwa, na chanda kili kinywani!

Wasichana siwaachi, mkidhani mko wema
Hamjui haki zenu, mwanyamaza kikondoo
Kusema ndio au la. ni ngumu sana kwenu
Simameni kwa pamoja, mtetee haki zenu!

Simwambii mwafahamu, wanaume ni wajanja
Switi! Supu! Darling!  Mwishowe tu kitandani
Miezi tisa hisabu, mmezidisha wawili
Ondoka na poteleya, toto mimi silijuwi!

Utalia na ulee, mtoto bila babake
Taumiya daima, ulipenda starehe
Mbona sina dadi yangu? Tauliza baadaye
Tamwambiya ni nani, motto umpendaye?

Shairi langu ni refu, tena halina kifani
Muda wangu umekwisha, MC anasema
Muda kwisha si hoja, nyie nd’o mtasema
Nangoja uamuzi wenu: Nende au nendelee?

                        @2000 Martinokariithi

No comments:

Post a Comment